Magazeti Manne Yafunguliwa Katika Tanuri Ya Moto

Wamiliki wa magezi yaliyokuwa yamefungiwa kuchapisha habari nchini Tanzania, siku ya leo wanasherekea kufunguliwa kwa magazeti hayo na kurudishiwa leseni zao rasmi kuendelea kuchapisha magazeti na kuhabarisha wananchi.

Magazeti hayo yalifungiwa katika vipindi tofauti tofauti huku yakisadikika kukiuka sheria mbalimbali za vyombo vya habari, ikiwa ni pamoja na kudaiwa kuchapisha habari za uchochezi zilizolenga kueneza chuki miongoni mwa wananchi.

Leo februari 10, 2022 waziri wa habari Nape Mnauye amekabidhi rasmi leseni nne za magazeti yaliyokuwa yamefungiwa kuchapisha habari, ikiwa ni miongoni mwa jitihada za serikali ya awamu ya sita kuimalisha uhuru wa vyombo nchini.

Ikumbukwe kuwa sheria zilizotumika kuyafungia magazeti hayo na zinalalamikiwa na wadau wa tasinia ya habari kuwa zinaminya uhuru wa vyombo vya habari nchini, bado zinaenelea kutumika, hivyo kufungulia magazeti ikiwa bado sheria kandamizi zinaendelea kufanya kazi ni ishara kwamba wenda yasidumu kwa muda mrefu na badala yake yakafungiwa kwa mara nyingine,

Magazeti yaliyofunguliwa

Miongoni mwa magazeti yaliyofunguliwa siku ya leo ni pamoja na gazeti la Mwanahalisi, Tanzania Daima, Mawio pamoja na Gazeti la mseto ambayo yote kwa pamoja kwa vipindi tofauti tofauti yalidaiwa kukiuka misingi na sheria za vyombo vya habari nchini.

Gazeti la Tanzania Daima lilifungiwa tangu june 23, 2020 huku wakidaiwa kuandika habari za uchochezi ikiwepo habari yenye kichwa kilichosomeka “Lisu, Ndugai jino kwa jino” lakini kabla ya hapo pia serikali ilikuwa imeishatoa onyo kadhaa kutokana na gazeti hilo kuandika habari kadha wa kadha ambazo zilidaiwa kuvunja kanunu na sheria ya habari nchini.

Mchakato wa kufungulia Magazeti

Mchakato huu wa kuvifungulia vyombo vya habari ulianza mara tu baada ya Rais Samia Suluhu Hassan kuingia madarakani, wakati akitoa hotuba yake alitoa maelekezo vyombo vya habari vifunguliwe lakini badala yake vilifunguliwa vyombo pekee ambavyo vinarusha maudhui yake kwa njia ya mtandao yaani (Online Channels).

Jambo hili lilizua gumzo kubwa sana mitandaoni na hivyo kutolewa tamko kuwa, serikali inabidi ikae na wamiliki wa vyombo hivyo ili kupitia upya mashitaka ya vyombo hivyo na kuangalia namna ya kurejesha leseni.

Mchakato huo uliongozwa na aliyekuwa waziri wa habari, sanaa na utamaduni Innocent Bashungwa ambaye kwa sasa anahudumu katika ofisi ya Rais TAMISEMI akiwa Waziri wa TAMISEMI, na waziri Nape Mnauye aliyechukua nafasi yake siku ya leo amefanikisha kurejeshwa kwa leseni za magazeti hayo.

Je kufunguliwa kwa magazeti ni ishara ya kurejea kwa uhuru wa vyombo vya habari nchini?

Baada ya taarifa ya kufunguliwa kwa magazeti hayo, kumekuwa na mijadala mbalimbali ya wadau wa habari pamoja na wanaharakati, huku wakionesha kufurahishwa na kitendo hicho lakini dukuduku lao bado lipo katika sheria kandamizi amazo zinatumika,

Kupitia ukurasa wa twiter mwanahabari pamoja na mchambuzi wa masuala ya kisiasa Ansbert Ngurumo ameeleza kuwa ni kweli magazeti yamefunguliwa na ni hatua nzuri , lakini huyo huyo aliyeyafungia leo ndio anaweza kuyafungia tena kesho na kuweka wazi kuwa lazima kuondoa kwanza kiini cha tatizo.

“Mithili ya mfuga kuku na banda lake, tusipoondoa kiini cha tatizo tukashangilia mambo madogo haya kama mazuzu, hatimaye hayatafungwa magazeti bali tutafungwa sisi wenyewe”

Hoja hii ina maana ya kuwa, serikali inaweza kufika hatua ambayo, badala ya kufungia magazeti bali inawafunga waandishi wanaandika magazeti hayo na matokeo yake inasababisha hofu miongoni wa waandishi na kuondoa dhana halisi ya vyombo vya habari katika kufichua maovu.

Sheria Kandamizi kwa vyombo vya habari nchini

Sheria ya vyombo vya habari ya mwaka 2016, inatajwa kuwa sheria tishia kwa vyombo vya habari na wanahabari kutokana na kuweka mipaka kwa vyombo vya habari katika kuripoti matukio mbalimbali.

Ni kupitia sheria hiyo magazeti pamoja na vyombo vyahabari vya mitandao vinafungiwa pamoja na kutozwa faini na kutakiwa kuomba msamaha kwa muda kadhaa, Ni kweli kuna wakati waandishi na watangazaji wanajisahau lakini pale ambapo kinachoripotiwa kina ukweli ndani yake inabidi kipewe nafasi ya kufanyiwa uchunguzi na sio kufungia chombo cha habari kisa tu kimegusa tabaka tawala.

Chanzo: Mkutano wa Waziri wa Habari, Bbc Swahili pamoja na TBC1

Enjoyed this article? Stay informed by joining our newsletter!

Comments

You must be logged in to post a comment.

About Author

JOURNALIST